Na: Nassoro Rashid - Mkingadc Habari
Mkuu wa wilaya ya Mkinga Mhe. Gilbert Kalima ametoa wito kwa Mashirika yasiyo ya Kiserikali kushirikiana na Serikali katika kupiga vita vitendo vya ukatili wa kijinsia, matumizi ya madawa ya kulevya, ubakaji pamoja na ulawiti kwa jamii.
Mhe. Kalima ametoa wito huo Agosti 21, 2024 wakati alipokuwa akifungua Jukwaa la Mashirika yasiyo ya Kiserikali lililofanyika katika ukumbi wa Halmashauri.
Akizungumza kwa msisitizo Mkuu wa wilaya amesema kazi ya kupiga vita matendo yanayokiuka maadili ni jukumu la wote hivyo ameroa wito kwa Mashirika hayo kushirikiana na serikali ili kuijenga Mkinga isiyo na tabia za ukiukwaji wa maadili.
"Kumekuwa na matukio mbalimbali ya ukatili wa kijinsia, matumizi ya madawa ya kulevya, ubakaji na ulawiti yanayokiuka sheria za nchi, naomba tuongeze nguvu katika kusimamia suala zima la maadili ili kuijenga jamii yetu katika misingi iliyo bora na inayomcha Mungu, tupige vita kwa nguvu zetu zote ili kuondokana na tabia hizi". Alisema Mhe. Kalima.
Aidha Mhe. Kalima amesema hawawezi kupuuza juhudi na kazi kubwa zinazofanywa na mashirika hayo katika kuwafikia Wananchi kupitia sekta mbalimbali na kuahidi kuwa serikali ipo tayari na itaendelea kushirikiana nao ili kuhakikisha dhana ya maendeleo endelevu inatafsiriwa ipasavyo kwa wananchi.
"Nipende kuchukua nafasi hii kuwapongeza sana kwani nyinyi mmekuwa wadau wakubwa wa maendeleo katika wilaya yetu, tupo tayari kuendeleza ushirikiano huu ili kuhakikisha malengo ya kazi zilizopangwa kwa wilaya ya Mkinga zinafanikiwa". Alisema Mhe. Kalima.
DC Kalima amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira mazuri kwa wadau wa maendeleo yakiwemo mashirika hayo kwenye utekelezaji wa shughuli zao ikiwa ndio ishara nzuri na upendo wa Mhe. Rais kwa Wananchi wake wa Tanzania.
Jukwaa hilo hufanyika kila mwaka kisheria ambapo viongozi wa Mashirika yasiyo ya kiserikali pamoja na wataalam hukaa pamoja na kujadili uwasilishwaji wa taarifa za utendaji kazi na kubadilishana uzoefu, pia kupata fursa ya kujadili mafanikio makubwa ambayo yamepatikana kupitia juhudi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali wa maendeleo.
#Kaziiendelee
Kasera, Tanga -HorohoroRoad
Postal Address: P O Box 6005 Tanga
Simu: +255 755 443 326
Simu: +255 755 443 326
Barua Pepe: Info@mkingadc.go.tz
Mkinga dc @ 2017