Na: Nassoro Rashid - Mkingadc Habari
Wito umetolewa kwa jamii ya wilaya ya Mkinga kuchukua tahadhari dhidi ya homa ya nyani ambao ni ugonjwa wa mlipuko unaosababishwa na kirusi aina ya Mpox.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa wilaya ya Mkinga Mhe. Gilbert Kalima Agosti 20, 2024 wakati akiongoza kikao cha Kamati ya Afya ya Msingi (PHC) kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa wilaya.
Kikao hicho kilichojumuisha Kamati ya Ulinzi na Usalama, Viongozi wa Dini, Kamati ya wataalam ya Halmashauri, Wataalam wa Afya, Wazee Maarufu pamoja na Maafisa Tarafa.
Akizungumza katika kikao hicho Mhe. Kalima amesema kila mtu kwa nafasi yake anapaswa kuchukua tahadhari kwa kutoa elimu kwa jamii ili kuhakikisha Wananchi wanajengewa uelewa wa kutosha ili kuepukana na ugonjwa huo.
"Niwaombe kila mmoja wetu kwa nafasi yake kuanzia Viongozi wa Dini, Vijiji, Kata, Kamati za ulinzi na Usalama, Madiwani, Walimu, Wataalam wa afya pamoja na Wananchi kwa umoja wetu kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huu, tunapaswa kutoa elimu hii kwa Jamii ili kujengeana uelewa zaidi kwani Mkinga ni moja ya Wilaya zilizopo mpakani hivyo tukishirikiana vizuri tutafanikiwa kuudhibiti". Alisisitiza Mhe. Kalima.
Aidha Mhe. Kalima amesema kwa pamoja wameazimia kuwa elimu iendelee kutolewa kuhusu dalili na namna ya kujikinga na ugonjwa kupitia wataalam wa afya, pili viongozi wa dini kutoa elimu kwa wananchi maeneo ya ibada, elimu kutolewa mashuleni ili wanafunzi wafikishe ujumbe huo kwa Wazazi na Walezi pamoja na matangazo kwa umma.
Kadhalika Halmashauri kuweka mikakati ya ujenzi wa zahanati ya Horohoro pamoja na kutenga bajeti ya dharula kwa ajili ya utayari wa udhibiti mzuri wa ugonjwa huu.
Naye Kaimu Mganga Mkuu Dkt. Castory Chuwa amesema virusi vya Mpox kawaida hushambulia panya au nyani na unaweza pia kumshambulia binadamu.
Pia ameongezea kuwa ugonjwa huu umetolewa taarifa katika nchi za Afrika ya kati na Magharibi na visa vingi katika nchi za kusini mwa jangwa la Sahara Afrika kutokana na uwepo wa mwingiliano wa wasafiri (Binadamu, Wanyama na bidhaa mbalimbali) kutoka mataifa mbalimbali.
#Kaziiendelee
Kasera, Tanga -HorohoroRoad
Postal Address: P O Box 6005 Tanga
Simu: +255 755 443 326
Simu: +255 755 443 326
Barua Pepe: Info@mkingadc.go.tz
Mkinga dc @ 2017