

Na: Nassoro Rashid – Mkinga

Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Mhe. Gilbert Sylvester Kalima, amesema serikali wilayani humo imejipanga kuanzisha mkakati shirikishi wa kuinua zao la korosho kwa kushirikiana na wananchi, viongozi wa vijiji na wataalamu wa kilimo, ili kuongeza uzalishaji na tija kwa wakulima.
Mhe. Kalima aliyasema hayo Septemba 30, 2025 wakati akiongoza ziara ya kamati ya ulinzi na usalama akiwa ameambatana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya, Ndugu Rashid Gembe, pamoja na kamati ya wataalamu kukagua miradi ya kimkakati inayotekelezwa katika wilaya hiyo.
Alisema korosho ni zao la kimkakati linaloweza kuchochea uchumi wa Mkinga, hivyo ipo haja ya kuweka mpango maalum wa kuwasaidia wakulima kuondokana na changamoto zinazowakabili, ikiwemo upatikanaji wa pembejeo bora, elimu ya kitaalamu ya kilimo bora na uhakika wa masoko.
“Tunataka mkakati huu uwe shirikishi, maana yake wananchi wenyewe washirikishwe tangu hatua za awali za kupanga hadi kutekeleza. Tukiwa na ushirikiano wa karibu kati ya serikali, wataalamu na wakulima, tutaweza kulifanya zao la korosho kuwa uti wa mgongo wa uchumi wa Mkinga,” alisema DC Kalima.
Aidha Mhe. Kalima alisisitiza umuhimu wa kutoa elimu kwa wakulima na wananchi kuhusu zao la korosho, akieleza kuwa baadhi yao wamekuwa wakiliacha zao hilo kutokana na mitazamo potofu na changamoto za muda mrefu zilizowahi kujitokeza.
“Tunataka mkakati huu usibaki kwenye karatasi pekee, bali uende sambamba na elimu ya mara kwa mara kwa wakulima wetu. Wengi wamekuwa wakiliacha zao hili wakidhani halina tija, kumbe tatizo ni ukosefu wa mbinu bora na maarifa ya kilimo cha kisasa. Tukiwapa elimu sahihi, mitazamo yao itabadilika na wataona thamani kubwa ya zao hili,” alisema DC Kalima.
Alibainisha kuwa elimu hiyo itatolewa kupitia maafisa ugani, mikutano ya vijiji, pamoja na vikundi vya wakulima ili kuhakikisha kila mkulima anafikiwa na kupata uelewa wa kutosha.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Rashid Gembe, alisema mpango huo utahusisha pia uhamasishaji wa matumizi ya miche bora ya kisasa badala ya mashamba pori yaliopo sasa na kuimarisha usimamizi wa vyama vya ushirika ili kuhakikisha wakulima wananufaika moja kwa moja na mazao yao.
Mkakati huo unatarajiwa kuongeza uzalishaji wa korosho wilayani Mkinga na kuchochea mapato ya serikali na kaya, sambamba na kufungua fursa mpya za biashara kwa wananchi.
Ziara hiyo ilihusisha ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa ghala la korosho lenye uwezo wa kuhifadhi zaidi ya tani 10,000, kutembelea kikundi cha kinamama wachakataji wa mhogo Mtimbwani, wanufaika wa TASAF kijiji cha Tawalani, pamoja na maendeleo ya ujenzi wa soko la samaki Moa.
#mkingakaziinaendelea
Kasera, Tanga -HorohoroRoad
Postal Address: P O Box 6005 Tanga
Simu: +255 027-2660501
Simu: +255 684 625 299
Barua Pepe: Info@mkingadc.go.tz
Mkinga dc @ 2017