Na: Nassoro Rashid - Mkingadc Habari
Leo Agosti 13, 2024 Mkuu wa wilaya ya Mkinga Mhe. Gilbert Kalima amezindua kampeni ya umezeshaji wa kingatiba za magonjwa ambayo hayapewi kipaumbele ikiwemo ya usubi.
Kampeni hii ni mwendelezo wa zoezi lililofanyika mwezi Februari mwaka huu ikiwa ni kukamilisha zoezi hilo ambapo kila mwaka kingatiba za usubi hutolewa kwa awamu mbili.
Aidha katika uzinduzi huo Mhe. Kalima ameihasa jamii ya wilaya ya Mkinga kuungana katika kumeza kingatiba hizo ili kuweza kuondokana na athari zinazoweza kusababishwa na ugonjwa huo ikiwemo minyoo, upofu na matatizo ya ngozi.
"Niwaombe Wananchi wa Mkinga kuhakikisha wanashirikiana na Wataalamu wetu wanaopita nyumba kwa nyumba kwa ajili ya umezeshaji wa kingatiba hizi ili kuepuka madhara yanayotokana na usubi, kwani usikivu wao unatupa imani kwamba tutafanikisha kampeni hii kwa matokeo mazuri". Alisema Mhe. Kalima
Sambamba na hilo amesema kuwa zoezi hili linawahusu Watu wote wenye umri kuanzia Miaka 5 na kuendelea na litafanyika nyumba kwa nyumba kupitia Watalaam waliopewa mafunzo maalum.
Naye Mganga Mkuu wa wilaya Dkt. Salvio Wikesi amesisitiza kuwa kingatiba hizi ni salama na hazina madhara yoyote kwani unapopatiwa kingatiba hizi husaidia kutibu minyoo ya aina yote, kuzuia matatizo ya ngozi na upofu.
Kampeni hii imeanza rasmi Agosti 12 na inatarajiwa kutamatika Agosti 18, 2024 hivyo jamii inahimizwa kuunga mkono katika kuhakikisha wanapatiwa kingatiba hizi katika nyumba zao.
JAMII ILIYOBORA NI JAMII INAYOJALI AFYA YAKE.
#Kaziiendelee
Kasera, Tanga -HorohoroRoad
Postal Address: P O Box 6005 Tanga
Simu: +255 755 443 326
Simu: +255 755 443 326
Barua Pepe: Info@mkingadc.go.tz
Mkinga dc @ 2017