Na: Nassoro Rashid - MDC Habari
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian ameipongeza Halmashauri ya wilaya ya Mkinga kwa kupata hati safi ya ukaguzi wa hesabu za serikali kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Ameyasema hayo leo Juni 13, 2024 wakati akihutubia katika mkutano wa baraza maalumu la hoja la madiwani uliofanyika katika ukumbi uliopo Halmashauri ya wilaya ya Mkinga.
Mhe. Dkt. Batilda ametumia nafasi hiyo kuwapongeza viongozi pamoja na wataalamu kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuhakikisha Halmashauri hiyo inapiga hatua kimaendeleo katika nyanja mbalimbali huku akiwapongeza kwa kupata hati safi ya mkaguzi wa hesabu za serikali.
"Sisi kwa mkoa wetu kati ya Halmashauri 11, 10 zimepata hati safi yani hati inayoridhisha ikiwemo na Halmashauri ya wilaya ya Mkinga, hongereni sana, nawapongeza Mhe. Mwenyekiti, Mkurugenzi, Wah. Madiwani pamoja na Wataalamu kwa kazi nzuri ambayo mmefanya na kufanikiwa kupata hati safi kwa mwaka wa fedha 2022/2023". Alisema Mhe. Dkt. Batilda
Kadhalika Mkuu huyo wa Mkoa amesema kuwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akitoa fedha nyingi sana kutekeleza miradi ya maendeleo hivyo ametoa wito kwa viongozi na Wataalamu kuendelea kusimamia ipasavyo na kuhakikisha fedha hizo zinafanya kazi zinazokusudiwa.
Sambamba na hayo Mhe. Batilda ameelekeza kuanzishwa kwa kituo maalum cha utoaji wa huduma za serikali (One Stop Centre) kwenye kila Halmashauri ili kusaidia utoaji wa huduma mbalimbali za mfumo mtandao ikiwemo wa TAUSI ili kusaidia upatikanaji wa leseni za biashara na huduma zingine kwa haraka.
Katika hatua nyingine Mhe. Batilda amekemea vikali vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto na kuitaka jamii kwa umoja wao kutoa ushirikiano na kuungana na serikali katika kuhakikisha wahusika wanachukuliwa hatua za kisheria kwa wakati.
#kaziiendelee
Kasera, Tanga -HorohoroRoad
Postal Address: P O Box 6005 Tanga
Simu: +255 755 443 326
Simu: +255 755 443 326
Barua Pepe: Info@mkingadc.go.tz
Mkinga dc @ 2017