Na. Nassoro Rashid
MDC Habari
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe.Prof.Adolf Mkenda (Mb) kwa kuambatana na mgeni wake Rais wa Mfuko wa ABBOTT Duniani Bi. Melissa Brotz Julai 12, 2023 wamezindua mradi mkubwa wa ukarabati na uboresha wa miundombinu ya Shule ya Sekondari Mapatano iliyopo wilaya ya Mkinga.
Mara baada ya uzinduzi Mhe.Waziri Mkenda amesema mradi huo unaofadhiliwa na Mfuko wa Abbott utagharimu zaidi ya
shilingi Bilioni 8.9 hadi kukamilika kwake na kuifanya shule ya Mapatano kuwa ya mfano Mkoani Tanga.
"Mradi huu unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 12 ambapo utahusisha majengo zaidi ya thelathini (30), ni imani yangu kwamba shule hii inakwenda kuwa ya mfano mkoa wa Tanga kutokana na maboresho yake pamoja na kujengwa kwa miundombinu ya madarasa yote yaliyopo sambamba na kujenga madarasa mapya ya kidato cha tano na sita, maabara za kisasa, mabweni, viwanja vya michezo pamoja na ujenzi wa nyumba za walimu". Alisema Mhe. Waziri Mkenda.
Naye Rais wa Mfuko wa Abbott Duniani Bi.Melissa amesema wanafahamu kwamba kuboresha miundombinu ya elimu ni sehemu ya kuimarisha
maendeleo yake hivyo hawatoacha kuendelea kufadhili miradi ya elimu ili maono ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yatimie ya kuhakikisha Wananchi wote wanapata elimu bora pamoja na kuboresha maisha yao kwa kuleta maendeleo nchini.
Sambamba na hayo Mkuu wa Wilaya ya Mkinga Mhe. Kanali Maulid Hassan Surumbu ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe.Waziri Kindamba alisema,
"Uwepo wa wadau mbalimbali wa maendeleo katika Mkoa wa Tanga na leo Wilaya ya Mkinga ni matunda ya kazi nzuri inayofanywa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuifungua Tanzania, hivyo hatuna budi kuendelea kumuunga mkono na kumshukuru kwa jitihada hizi
ambazo zinaendelea kuinufaisha wilaya hii kupitia uboreshwaji wa miundombinu ya elimu lakini pia na sekta nyingine kwa ustawi mpana wa maendeleo ya Wananchi". Aliongezea Mhe. Kanali Surumbu.
Shughuli hiyo pia ilihudhuriwa na Wajumbe wa Kamati ya Usalama Wilaya, Mwenyekiti wa CCM Wilaya, Mbunge wa Jimbo la Mkinga ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii kwa sasa Mhe.Dunstan Kitandula, Mwenyekiti wa Halmashauri, Diwani wa Kata ya Mapatano na Viongozi mbalimbali wa Wilaya,Kata na Kijiji.
Kasera, Tanga -HorohoroRoad
Postal Address: P O Box 6005 Tanga
Simu: +255 755 443 326
Simu: +255 755 443 326
Barua Pepe: Info@mkingadc.go.tz
Mkinga dc @ 2017