Na: Nassoro Rashid
MDC Habari
Kaimu Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya wilaya ya Mkinga Bi. Elizabeth Malali Novemba 01, 2023 amekutana na Maafisa Maendeleo Jamii kutoka katika Kata 18 ikiwa ni kuendeleza mikakati ya uimarishaji wa utendaji kazi pamoja na kuongeza nguvu ya ukusanyaji wa marejesho ya mikopo ya 10% iliyotokana na mapato ya ndani.
Akizungumza wakati wa kikao hicho Bi. Elizabeth amesema kupitia idara hiyo wameweza kufanikiwa kutekeleza shughuli mbalimbali ikiwemo uhamasishaji wa Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu kupitia Dawati la uwezeshaji Wananchi kiuchumi hususani katika Mikopo ya 10%.
"Tangu kuanza kwa mikopo hii Halmashauri imefanikiwa kutoa shilingi 652,004,381 kupitia mapato yake ya ndani kwa makundi 145, hadi sasa tumefanikiwa kurejesha shilingi 258,391,943 na bakio la deni ni shilingi 375,612,438, ambapo kati ya deni hilo shilingi 68,290,638 ni fedha ya vikundi vilivyopo nje ya mkataba na shilingi 286,321,800 ni fedha zilizopo ndani ya mkataba, dhamira kubwa ya serikali ni kuhakikisha mikopo hii inarejeshwa, hivyo sisi kama Idara tumeendelea kufanya jitihada za ufuatiliaji katika kipindi cha Robo hii na tumeweza kukusanya shilingi milioni 18, 000,000 kwa vikundi vilivyo nje ya mkataba". Alisema Bi. Elizabeth
Aidha Bi. Elizabeth amesema kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wameweza kuwapata wanufaika 6231 kupitia kuunda vikundi vya kuweka akiba na kuwekeza 294 kwa vijiji 84 ambapo Wanachama katika vikundi hivyo ni 3766 ikiwemo Wanawake 3410 na Wanaume ni 356.
"Lengo la utekelezaji huu ni kuhakikisha kwamba uwezeshaji Wananchi kupitia miradi ya TASAF unaleta matokeo chanya kwenye familia katika kuongeza kipato, na lengo la kuunda vikundi kwa wanufaika huwasaidia kubuni miradi mbalimbali pamoja na kuweka akiba za fedha zao ili kuona manufaa ya fedha hizo katika kuwainua kiuchumi." Alisema Bi. Elizabeth
Pia ameongezea kuwa kikao hicho kililenga kuangalia miongozo mbalimbali inayotolewa na serikali ikiwemo uundaji wa Mabaraza ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Mabaraza ya Watoto na miongozo mingine ya Idara ili kuhakikisha Maafisa hao ngazi ya Kata Wanaunda mabaraza hayo ili Wananchi waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo.
Naye mratibu wa TASAF wilaya Ndugu. Benson Ogada amewasisitiza maafisa maendeleo kata kuhakikisha Mashirika yote yaliyopo kwenye Kata zao yatambulike kuanzia ngazi hiyo mpaka Wilaya lakini pia mpango kazi wa mashirika hayo ufikishwe kwa maafisa hao ili waweze kujua kazi wanazojihusisha nazo kwa maslahi mapana ya ustawi mzuri wa jamii ya Wanamkinga.
Kikao hicho ni muendelezo wa vikao vya idara kila ifikapo robo mwaka vikiendelea kuwa na dhamira chanya ya kuhakikisha jamii inaendelea kuhamasishwa katika shughuli za kimaendeleo kupitia tathmini ya pamoja ya utendaji kazi ili kuendeleza mikakati ya kuimarisha shughuli mbalimbali za idara katika kuhakikisha dhana ya maendeleo ya jamii inafikiwa kwa vitendo.
Kasera, Tanga -HorohoroRoad
Postal Address: P O Box 6005 Tanga
Simu: +255 027-2660501
Simu: +255 684 625 299
Barua Pepe: Info@mkingadc.go.tz
Mkinga dc @ 2017