Na: Nassoro Rashid - Mkingadc Habari
Mkuu wa wilaya ya Mkinga Mhe. Gilbert Kalima amewataka wazazi na walezi kuhakikisha wanaunga mkono jitihada za serikali katika kuendeleza agenda ya lishe mashuleni ili kuimarisha uwezo wa watoto kuweza kufanya vizuri katika masomo yao.
Mhe. Kalima ameyasema hayo wakati akiongoza kikao cha utekelezaji wa shughuli za lishe wilaya ya Mkinga Agosti 13, 2024 kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Wilaya kukamilisha robo ya nne ya mwaka wa fedha 2023/2024.
Aidha ametumia nafasi hiyo kuikumbusha jamii ya Mkinga kuendelea kushirikiana katika utekelezaji wa shughuli za lishe kuanzia ngazi ya msingi hadi wilaya huku akiitaka jamii, viongozi wa ngazi ya vijiji, kata na wilaya kushirikiana kwa dhati kumuunga mkono Mhe. Rais Dkt. Samia katika utekelezaji wa agenda ya lishe kwa vitendo.
"Niwakumbushe viongozi wenzangu kuanzia ngazi ya vijiji, kata hadi wilaya kuwa agenda ya lishe ni ya kudumu, hivyo tunapaswa kushirikiana na jamii ili kuhakikisha tunaifanikisha agenda hii kwa vitendo kupitia uhamasishaji ili jamii iweze kuielewa zaidi na kuleta matokeo chanya." Alisisitiza Mhe. Kalima
Sambamba na hilo Mkuu huyo wa wilaya amesisitiza kila kaya kuweka umuhimu wa ujenzi na matumizi ya vyoo safi na salama ili kuepuka magonjwa ya mlipuko huku akiongeza kuwa matumizi sahihi ya vyoo safi ni msingi imara wa ustaararabu kwa mwanaadamu.
Katika hatua nyingine ametoa wito kwa Wananchi kuacha tabia ya kuanika vyakula kando kando ya barabara kwani ni hatari kiafya kutokana na kupokea sumu inayotokana na moshi wa vyombo vya moto vinavyotumia barabara hizo.
#Kaziiendelee
Kasera, Tanga -HorohoroRoad
Postal Address: P O Box 6005 Tanga
Simu: +255 027-2660501
Simu: +255 684 625 299
Barua Pepe: Info@mkingadc.go.tz
Mkinga dc @ 2017