Na: Nassoro Rashid - MDC Habari
Kauli hiyo imesemwa Januari 08, 2024 na Mkuu wa wilaya ya Mkinga Mhe. Kanali Maulid Hassan Surumbu mara baada ya kutembelea shule za msingi, awali na sekondari kuona mapokeo ya wanafunzi katika muhula mpya wa masomo ulioanza siku ya Jumatatu ya wiki hii.
Katika ziara yake hiyo Mhe. Surumbu amesema mwamko wa wanafunzi kuhudhuria kwenye shule hizo umekuwa ni mkubwa sana kwa siku ya kwanza hivyo ameendelea kutoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha kila mtoto mwenye sifa anapelekwa shule.
"Mkinga ina Shule za Msingi 87 na Sekondari 17, shule zote zimefunguliwa wiki hii, tunashukuru mwitikio wa wanafunzi kwa mwaka huu umekuwa ni wa kuridhisha kutokana na uhamasishaji shirikishi kutoka ngazi ya Kitongoji hadi Wilaya, malengo ya Wilaya ni kuhakikisha kila mtoto aliyefikia umri wa kuanza Shule anaandikishwa na si vinginevyo, hivuo Mtoto mwenye umri wa miaka 5 aandikishwe shule ya Awali na wa miaka 6 Darasa la Kwanza" alisema Mhe. Kanali Surumbu
Aidha Mkuu huyo wa wilaya ametoa wito kwa viongozi kuanzia ngazi ya Tarafa hadi Vijiji kupita kila nyumba ili kuona kama kuna mtoto hajapelekwa shule hatua za kinidhamu zichukuliwe kwa mzazi au mlezi wa mtoto huyo.
"Wito mwingine natoa kwa viongozi wa Tarafa, Kata, Vitongoji na Vijiji kuhakikisha wanapita nyumba kwa nyumba ifikapo Tarehe 10,2024, kila mzazi mwenye mtoto ambaye anastahili kwenda shule aende shule na kama hafanyi hivyo hatua za kinidhamu zichukuliwe kwa mzazi husika, na asibaki mtoto nyumbani kwa kisingizio cha mwanafunzi amekosa sare, apelekwe shule ili aanze masomo pamoja na wenzake". Alisisitiza Mhe. Surumbu.
Pia Mhe. Kanali Surumbu amesema shule ambazo zimeendelea kujengwa kwenye wilaya ya Mkinga kupitia miradi mbali mbali takribani 19 ikiwemo pochi ya mama, Boost na miradi mingine inayowezeshwa na Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imejengwa kwa kuzingatia huduma ya watoto wenye mahitaji maalumu hivyo pia amewataka wazazi kuwapeleka shule watoto hao ili waweze kupata elimu.
"Watoto wote wenye mahitaji maalum nao wanatakiwa kuripoti kwenye shule hizi, walimu kwa ajili ya kuwafundisha wameshaandaliwa na wapo tayari, kila mzazi au mlezi anayeishi na mtoto mwenye mahitaji maalum asikae naye nyumbani na asimfiche, ahakikishe anamtoa ili aweze kupata haki yake ya elimu". Aliongezea Mhe. Surumbu..
Elimu imekuwa ni msingi muhimu wa maisha kwa binaadamu kwani imeweza kusaidia sana kwa kiasi kikubwa kuijenga Tanzania ya leo na Dunia ya sasa tunayoiona hivyo wananchi hususani wazazi na walezi wanaendelea kuhimizwa kuhakikisha wanawapa kipaumbele watoto wao kupata elimu ili ije kuinufaisha jamii kimaendeleo kadhalika kuimarisha ustawi bora wa Nchi yetu.
Kasera, Tanga -HorohoroRoad
Postal Address: P O Box 6005 Tanga
Simu: +255 755 443 326
Simu: +255 755 443 326
Barua Pepe: Info@mkingadc.go.tz
Mkinga dc @ 2017