Na: Nassoro Rashid – Mkinga
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga, Ndugu Rashid Gembe, amewakumbuka walimu wenye mahitaji maalum kwa kuwakabidhi vifaa vya TEHAMA vikiwemo kompyuta mpakato na kishikwambi, hatua inayolenga kuwawezesha kitaaluma na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya ufundishaji shuleni.
Akizungumza mara baada ya makabidhiano hayo, Mkurugenzi huyo amesema kuwa vifaa hivyo vitakuwa chachu kwa walimu hao katika kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji, hali itakayowasaidia kutekeleza majukumu yao ya kila siku kwa ufanisi zaidi.
“Ni matumaini yangu kuwa vifaa hivi vitaongeza ufanisi katika ufundishaji na ujifunzaji ili watoto wetu waendelee kupata elimu bora kupitia matumizi ya nyenzo za kisasa. Nimshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Elimu kwa kuwezesha upatikanaji wa vifaa hivi,” alisema Mkurugenzi Gembe.

Naye Mwalimu Ashura Mohamed Kameka wa Shule ya Msingi Maramba B amesema kuwa kompyuta mpakato aliyokabidhiwa itamsaidia kwa kiasi kikubwa katika shughuli za ufundishaji na ujifunzaji, hivyo kurahisisha utendaji kazi wa kila siku. Aidha, ameushukuru uongozi wa Halmashauri kupitia Idara ya Elimu Msingi na Awali kwa kuwajali walimu wenye mahitaji maalum.
Kwa upande wake, Mwalimu Yahaya Said Chaya wa Shule ya Msingi Ng’ombeni amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwakumbuka walimu wenye mahitaji maalum kwa kuwapatia vifaa hivyo, akisema vitawarahisishia kazi ya ufundishaji na kuongeza ufanisi katika utoaji wa elimu.
Hatua hiyo inaonesha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuimarisha sekta ya elimu kwa kuhakikisha walimu wote, wakiwemo wenye mahitaji maalum, wanapata nyenzo muhimu za kufanyia kazi katika mazingira rafiki na jumuishi, jambo linalochangia kuboresha ubora wa elimu na kufanikisha malengo ya maendeleo ya elimu nchini.
Kasera, Tanga -HorohoroRoad
Postal Address: P O Box 6005 Tanga
Simu: +255 027-2660501
Simu: +255 684 625 299
Barua Pepe: Info@mkingadc.go.tz
Mkinga dc @ 2017