Na: Grace Melleor – Mkinga
Kikao cha tathmini ya elimu kilichowakutanisha wadau mbalimbali wa sekta hiyo kimefanyika leo Machi 2, 2026 katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga, Mkoa wa Tanga, kikilenga kuibua mikakati mipya ya kuleta mageuzi ya ubora wa taaluma na kuinua viwango vya ufaulu kwa wanafunzi wilayani humo.
Akifungua kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Gilbert Kalima, amesema tathmini hiyo ni hatua muhimu katika safari ya maboresho ya elimu, kwani inatoa nafasi ya kuchambua mafanikio, kubaini changamoto na kuweka mikakati ya pamoja ya kuimarisha taaluma.
Amesisitiza kuwa mageuzi ya elimu hayawezi kupatikana bila ushirikiano wa wadau wote wakiwemo walimu, wazazi, viongozi na jamii kwa ujumla, akibainisha kuwa elimu bora ni msingi wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
“Kupitia kikao hiki tunataka kuona mabadiliko ya kweli katika ubora wa taaluma. Tujadili kwa uwazi changamoto zilizopo na tupate suluhu za kudumu kwa manufaa ya wanafunzi wetu,” amesisitiza Mhe. Kalima.
Kwa upande wake, Afisa Elimu Awali na Msingi (W), Ndugu Omari Mashaka, amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026 jumla ya Shilingi 982,507,846 zimetumika kutekeleza miradi ya maendeleo ya elimu, ikiwemo ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya shule. Amesema uwekezaji huo umeweka mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia, hatua inayochochea mageuzi ya taaluma.
Naye Afisa Elimu Sekondari (W), Bi. Mary Sanga, ameeleza kuwa Halmashauri imeongeza idadi ya shule za sekondari kutoka 15 mwaka 2023 hadi kufikia 21 mwaka 2026. Aidha, walimu wapya 37 wa masomo ya Sayansi, Lugha, Sanaa na Biashara wamepokelewa, jambo linalotarajiwa kuongeza ufanisi wa ufundishaji na kuimarisha matokeo ya wanafunzi.
Mdhibiti Ubora wa Elimu (W) Bi. Rosemary Thoran amebainisha kuwa tathmini ya matokeo ya mitihani ya Taifa kwa mwaka 2025 inaonesha mwelekeo chanya, ambapo ufaulu wa Darasa la IV umeongezeka kwa asilimia 1.5 na Kidato cha Nne kuongezeka kwa asilimia 2 kutoka asilimia 91.4 mwaka 2024 hadi asilimia 93 mwaka 2025.
Ameeleza kuwa ongezeko hilo ni matokeo ya juhudi za pamoja za walimu, wanafunzi na wadau wa elimu.
Kikao hicho kilichobeba kaulimbiu isemayo “Elimu Bora kwa Mtoto ni Jukumu Letu Sote” kinatajwa kuwa chachu ya mageuzi ya ubora wa taaluma katika Wilaya ya Mkinga, huku mipango ikiwekwa ya kuendeleza tathmini za mara kwa mara ili kuhakikisha maboresho yanakuwa endelevu na yenye matokeo chanya kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla.

Kasera, Tanga -HorohoroRoad
Postal Address: P O Box 6005 Tanga
Simu: +255 027-2660501
Simu: +255 684 625 299
Barua Pepe: Info@mkingadc.go.tz
Mkinga dc @ 2017